Beki wa Klabu bingwa nchini Guinea Horoya AC Mohamed Fofana ametoa kauli ya kuumizwa na Kiungo kutoka Zambia Clatous Chotta Chama, ambaye alikuwa mwiba katika mchezo wa Mzunguuko watano wa Kundi C, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Simba SC iliikaribisha Horoya AC Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam juzi Jumamosi (Machi 18), na kuibuka na ushindi wa 7-0, huku Mzambia huyo akipiga Hat Trick.
Fofana ambaye ni mrefu aliyekuwa katika ukuta wa Horoya AC wakati kikosi chao kikipata aibu nzito Barani Afrika amesema kama kuna mtu aliwavuruga katika mchezo huo basi ni kiungo huyo.
Amesema Chama ni mchezaji hatari sana wa Simba SC na alifanya kazi kubwa ya kuwavuruga katika eneo la Ulinzi na hata Kiungo, na kuiwezesha timu yake kupata ushindi mnono ikiwa nyumbani
“Nadhani yule aliyevaa jezi namba 17 (Chama) ni mchezaji hatari sana amesababisha matatizo makubwa sana kwenye eneo letu la ulinzi na hata katikati.”
“Alikuwa na mbio ambazo tulishindwa kumdhibiti vizuri, lakini kitu kibaya zaidi ni utulivu wake anapokuwa na mpira, hana papara wala hachezi kwa presha kama wenzake, tumelazimika kukubali matokeo. Ukiangalia mabao yote aliyoyafunga utagundua utulivu wa akili yake, ameisaidia timu yake nafikiri kitu bora tumejifunza tutarudi kujipanga kwa mashindano yajayo.” Amesema Fofana
Chama yuko juu katika orodha ya wafungaji mabao wa Ligi ya Mabingwa Afrika Hatua ya Makundi akiwa na manne sawa na Makabi Lilepo wa Al Hilal ya Sudan.
Ushindi wa 7-0 dhidi ya Horoya AC umeiwezesha Simba SC kuungana na Raja Casablanca ya Morocco katika Hatua ya Robo Fainali ikifikisha alama 09 baada ya kucheza michezo mitano ya Kundi C.
Raja Casablanca imejikusanyia alama 13 zinzoiweka kileleni mwa msimamo wa Kundi C, huku Horoya AC ikibaki katika nafasi ya tatu kwa kuwa na alama 04 na Vipers SC inaendelea kuburuza mkia kwa kuwa na alama 02.