Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Ukimw Fatuma Toufiq ameiomba Serikali kuharakisha mchakato wa kuifanya Hospitali ya Magonjwa Ambukizi ya Kibong’oto kuwa Taasisi kamili mapema.
Toufiq ametoa kauli hiyo leo wakati wa ziara ya Kamati katika Hospitali ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi ya Kibongóto iliyopo Wilaya ya Siha Mkoa wa Kilimanjaro kuona hali ya utoaji wa huduma za tiba pamoja na ukaguzi wa miradi ya maendeleo.
“Mimi na Kamati hii tunasema kwamba jambo hili la Kibong’oto kuwa Taasisi tumelichukua na tutahakikisha tunaenda kuishauri Serikali kuharakisha mchakato wa kuifanya Hospitali hii kuwa taasisi kamili” Amesema Toufiq.
Aidha amewapongeza watumishi katika Hospitali hiyo kwa kuendelea kutoa huduma bora kwa wagonjwa na kusema kuwa Kamati hiyo itaendelea kuishauri Serikali kutoa kipaumbele kwa Hospitali ya Kibongóto na kuhakikisha huduma bora zinaendelea kupatikana hapa.
Akijibu hoja ya kwanini Hospitali ya Kibongóto bado haijawa Taasisi kamili, Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Afya Bw. Tumainieli Macha amesema kuwa Serikali ipo kwenye hatua za mwisho kuifanya Hospitali ya Kibongóto kuwa Taasisi kamili mara baada ya muundo pendekezwa kupitishwa na Mamlaka husika.
Macha ameitaja Hospitali ya Magonjwa ya Akili Milembe pamoja Hospitali ya Rufaa ya Kanda – Mbeya kuwa ni miongoni mwa Hospitali zinazotarajiwa kuwa Taasisi pamoja na Hospitali ya Kibongóto.
Naye Mkurugenzi wa Hospitali hiyo Dkt. Leonard Subi ameishukuru Kamati hiyo kwa kupokea ombi la Hospitali hiyo kuwa Taasisi na kusema kuwa watumishi katika Hospitali hiyo wanafanya kazi kwa bidii na hivyo kuwaachia watunga Sera hao kuridhia maombi ya Hospitali hiyo kuwa taasisi.