Hospitali tatu zimeshambuliwa leo magharibi mwa mji wa Kyiv na kwenye mji wa bandari wa Mariupol.
Mamlaka nchini Ukraine zinasema ndege za Urusi zimezishambulia hospitali hizo usiku wa kuamkia leo Alhamis Machi 10 huku juhudi za uokozi zikiendelea.
Mashambulizi hayo yamekuja kukiwa na matumaini ya kuwahamisha raia kutoka miji kadhaa iliyozingirwa, ukiwemo Mariupol, ambao hauna chakula, maji, wala umeme kwa siku kadhaa sasa.
Mji mwingine ulioshambuliwa kwa mabomu ni Zhytomyr wenye wakazi 260,000 ulio magharibi mwa mji mkuu, Kyiv.
Mji huo umezingirwa na majeshi ya Urusi kwa siku tisa sasa, huku maafisa wa mji wakisema kuwa wakazi wake 1,200 wameuawa na wafanyakazi wa kujitolea wameanza kuzika maiti kwenye makaburi ya pamoja kutokana na kujaa kwa maeneo ya kuzikia.
Mkuu wa mkoa wa Kyiv, Oleksiy Kuleba, alisema kupitia televisheni kwamba “jeshi la Urusi limeyageuza maisha kuwa jahanamu, ambapo watu wanajificha chini ya mahandaki mchana na usiku wakiwa hawana chakula, maji wala umeme.”