‘Hosteli’ za wanafunzi zinazofahamika kama ‘Hosteli za Magufuli’ za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) zimeanza kutumika kama karantini ya siku 14 kwa wasafiri wanaoingia nchini.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ameeleza hayo alipokuwa anakagua majengo na vyumba vya hosteli hizo zilizoko katika eneo la Ubungo, umbali mfupi kutoka katika majengo ya utawala ya Chuo hicho.

“Uamuzi huu ni kuhakikisha tunadhibiti mienendo ya wasafiri wanaoingia ndani ya nchi wanaowekwa karantini,” alisema Waziri na kurejea ripoti za baadhi ya watu kutoroka katika karantini jijini humo.

“Lengo ni kuhakikisha Watanzania wako salama dhidi ya virusi vya corona, tumeamua kuwaweka wasafiri wote katika eneo moja ambalo litakuwa linalindwa muda wote; na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa atasimamia kwa kushirikiana na Wizara yangu,” aliongeza.

Alieleza kuwa wasafiri wanaowekwa karantini haina maana kuwa ni wagonjwa, lakini hii ni kutokana na kuwa wametoka kwenye nchi ambazo zimekumbwa na virusi vya corona.

Alisema watapimwa na watakaobainika kuwa hawana virusi vya corona baada ya kipindi cha wiki mbili watakuwa huru kuelekea majumbani kwao na watakaobainika kuwa wagonjwa watapelekwa hospitalini.

Athumani Ajib: Thamani yake itaonekana
Niyonzima amkubali Balama Mapinduzi