Baada ya mshambuliaji na nahodha wa kikosi cha timu ya taifa ya Argentina Lionel Messi kuomba kupumzishwa kwa muda, gwiji wa soka kutoka nchini Bulgaria Hristo Stoichkov, ameingia hofu na kuhisi huenda timu ya taifa hilo ikapata wakati mgumu bila ya kuwa na mshambuliaji huyo.
Stoichkov ambaye aliitumikia FC Barcelona kuanzia mwaka 1996–1998, amesema imekua ghafla kwa Messi kufikia maamuzi hayo, kwani aliamini huenda angetumia muda huu kuwaongoza wenzake, ili kutumia makosa waliyofanya wakati wa fainali za kombe la dunia kama sehemu ya kujifunza kupitia michezo ya kimataifa ya kirafiki.
Amesema ni aghalabu kwa mchezaji mwenye manufaa ya taifa lake kufanya maamuzi kama hayo, na hadhani kama hatua aliyoichukua inaweza kuleta ustawi mzuri wa kikosi cha Argentina ambacho bado kinasumbuliwa na upepo mchafu.
Gwiji huyo ambaye aling’ara na kikosi cha Bulgaria wakati wa fainali za kombe la dunia za mwaka 1994 na kufanikiwa kuifikisha nchi yake katika nafasi ya nne ya michuano hiyo, akaenda mbali zaidi na kuhisi huenda Messi akatumia nafasi ya kupumzika, kuchukua maamuzi ya kustaafu rasmi kuitumikia Argentina.
Amesema kama itakua hivyo Argentina itapata wakati mgumu sana, na huenda ikashindwa kufunga bao hata moja katika michezo watakayocheza kwa kipindi cha miaka mitatu.
“Endapo Messi atastaafu kuitumikia timu yake ya taifa, kuna hatari ya wachezaji watakaobaki wakashindwa kufunga bao hata moja kwa kipindi cha miaka mitatu.” Alisema Hristo Stoichkov
“Huenda akauli yangu ikachukuliwa kama dhihaka, lakini ninaaminsha hali itakua ngumu zaidi, kwa sababu ushirikiano na uwepo wa mchezaji kama Messi katika kikosi cha Argentina ina manufaa makubwa, kama ilivyo kwa FC Barcelona.”
“Binafsi nisingependa hatua hiyo itokee, ninamsihi Messi asiwaache wenzake katika kipindi hiki kigumu, atambue anahitajika kwenye timu ili kufanikisha malengo na mipango inayokusudiwa na mashabiki wa soka wa Argentina.”
Tayari ombi la Messi la kuhitaji kupumzika katika kipindi cha mwaka 2018 kilichosalia limeshakubaliwa na viongozi wa chama cha soka nchini Argentina (AFA) pamoja na benchi la ufundi, hivyo hatokua sehemu ya kikosi kitakachocheza mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Colombia mwanzoni mwa mwezi ujao.
Mpaka sasa Lionel Messi ameshaitumikia timu ya taifa ya Argentina katika michezo 128 na kufunga mabao 65.