Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), kwa kushirikiana na wadau, wanahitaji haraka dola milioni 68 kwa ajili ya usaidizi na huduma za uokozi wa maisha ya ongezeko la wakimbizi 96,000 ambao wamekimbilia Uganda hadi sasa.
Mwakilishi wa UNHCR nchini Uganda, Matthew Crentsil ameyasema hayo alipokuwa akizungumza hii leo na waandishi wa habari katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini Geneva, Uswisi.
Amesema, wakimbizi kutoka Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo – DRC, wakiendelea kukimbia ghasia na kutafuta usalama nchini Uganda, na mwitikio wa kibinadamu unaongezwa hadi kufikia hatua ya mwisho.
Katika ombi la UNHCR na wadau 41 yakiwemo mashirika sita ya Umoja wa Mataifa, mashirika 25 ya kimataifa na 10 ya kitaifa yasiyo ya kiserikali wanatafuta fedha hizo ili pia kuwasaidia wakimbizi 150,000, huku wanaowasili wakiendelea kuingia.
Mwanzoni mwa mwaka 2022, Uganda ilikuwa tayari inawahifadhi zaidi ya wakimbizi milioni 1.5 na kuifanya kuwa moja ya nchi muhimu zaidi zinazohifadhi wakimbizi duniani na kubwa zaidi katika bara la Afrika.
Hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Agosti, UNHCR ilikuwa imepokea asilimia 38 tu ya mahitaji yake ya ufadhili ya 2022 ya dola za Marekani milioni 343.4, ili kukidhi mahitaji ya wakimbizi nchini Uganda, kama ilivyoamuliwa mwanzoni mwa mwaka wa 2022.