Kamati ya kudumu ya Bunge ya Afya na UKIMWI, imefanya ziara katika Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe na Hospitali ya Mkoa wa Dodoma na kukagua miradi iliyojengwa kupitia fedha za UVIKO.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dkt. Faustine Ndugulile akizungumza katika ziara hiyo amegusia changamoto za afya ya akili nchini, na kupongeza ujenzi wa miundombinu hiyo na mikakati iliyopo ya kuipandisha hadhi hospitali ya Mirembe kuwa taasisi.
Amesema, “naishauri Serikali kuboresha upatikanaji wa dawa za afya ya akili kwani hali ya upatikanaji wa dawa kwa sasa ni asilimia 30. Pia, iweke mikakati ya mafunzo kwa kada za afya ya akili na kuimarisha mfumo wa utoaji wa huduma hizo kuanzia ngazi za jamii hadi ngazi ya rufaa.”
Katika ziara hiyo iliyofanyika Juni 23, 2023 kamati ya Bunge ilifanikiwa kujionea maboresho makubwa ya miundombinu yaliyofanyika katika hospitali hizo, huku Dkt Ndugulile akiitaka Serikali pia kuanzisha ‘call centre’ kwa ajili huduma za dharura za ushauri na usaidizi wa haraka kwa wahitaji.