Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango amesema huduma jumuishi za fedha ni miongoni mwa vipaumbele vya Nchi pia ni lengo muhimu la Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 pamoja na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano.

Mmpango ameyasema hayo wakati akizindua Mpango wa Tatu wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Fedha wa 2023-2028, hafla iliofanyika katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania Jijini Dar es salaam na kudai kuwa huduma jumuishi za fedha ni nguzo muhimu inayopaswa kuzingatiwa kwa kuhakikisha watu wa makundi yote wanafikiwa.

Amesema, wataalam na wadau wa huduma jumuishi za fedha kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi wanatakiwa kuhakikisha wanaongeza kasi ya upatikanaji wa vitambulisho vya taifa ili kusaidia katika upatikanaji wa huduma rasmi za kifedha hususani kwa vijana.

Aidha, amewasihi watalaam hao kuhakikisha malengo yaliowekwa katika mpango huo wa tatu wa huduma jumuishi za fedha yanafikiwa kikamilifu ifikapo mwaka 2028 hususani kwa kuelekeza juhudi katika makundi ambayo hayajafikiwa ikiwemo watu wenye ulemavu, wakulima wadogo, wavuvi, vijana, wanawake na wafanyabiashara wadogo.

Makamu wa Rais pia amesema ni vema kuendelea na jitihada za kuimarisha ulinzi wa watumiaji wa huduma za kifedha dhidi ya uhalifu wa mtandaoni, ili kuwajengea wateja imani ya kuendelea kutumia huduma hizo huku akitoa rai ya kupunguzwa kwa gharama za kutumia huduma rasmi za kifedha pamoja na kuongeza wigo wa dhamana.

Amesema, hatua hiyo, itarahirahisisha upatikanaji wa mikopo huku akitoa wito wa kuongezwa na kurahisishwa kwa miundombinu ya malipo ya pamoja ili kuchochea matumizi ya huduma rasmi za fedha na kuhakikisha upatikanaji wa mawasiliano kwa wote ili kupunguza matumizi ya fedha taslimu.

Bil 4.5 zaanzisha huduma mpya ya upasuaji MOI
Ukuaji wa Teknolojia utaziathiri AZAKI - Dkt. Ndugulile