Ligi kuu ya soka Tanzania bara msimu wa 2015-16 imekwisha kwa kishindo huku Young Africans wakiibuka mabingwa kwa mara nyingine na kuna baadhi ya wachezaji walionyesha uwezo mkubwa wa kucheza soka kupitia klabu zao.

Kutokana na umahiri waliouonyesha kwa kipindi cha msimu mzima, mtandao huu unakuletea kikosi cha wachezaji 11 bora.

 1. Aishi Manula

Manula anastaili kuwa kipa bora wa ligi ya msimu wa 2015/16, kutokana na mchango mkubwa alioutoa kwa timu yake katika mashindano yote aliyoichezea timu hiyo msimu huu.

Manula ndiye kipa aliyeidakia Azam FC mechi nyingi za ligi kuliko msaidizi wake Mwadini Ali, lakini pia kipa huyo aliipa ubingwa wa Kombe la Kagame timu hiyo bila kufungwa hata bao moja na pia alifanya kazi kubwa ya kuokoa hatari nyingi kwenye lango la Azam ilipocheza na Esperance ya Tunisia kwenye michauano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

 1. Juma Abduli

Beki wa Young Africans anayetajwa kuwa mchezaji bora msimu huu kutokana na mchango wake kwenye kikosi cha Young Africans na hata timu ya taifa, mabao mengi yaliyofungwa na Amissi Tambwe na Donald Ngoma yametokana na krosi za Juma ambazo mara zote zimekuwa na matunda kutokana na utaalamu aliokuwa nao.

 1. Mohamed Hussein ‘Tshabalala’

Mchezaji bora wa mwezi Aprili wa klabu ya Simba ambaye licha ya kuwa na umbo dogo lakini amekuwa na mchango mkubwa kwenye kikosi cha Simba, beki huyo wa kushoto ameonyesha uwezo mkubwa wa kuwadhibiti washambuliaji wakorofi lakini pia ameonyesha uwezo wa kupanda mbele kupiga krosi nyingi ambazo zilisababisha hatari kwenye lango la timu pinzani.

 1. Andrew Vicent ‘Dante’

Mlinzi makini kwenye safu ya ulinzi ya timu ya Mtibwa Sugar ambaye amefanya vizuri msimu huu na kuisaidia timu yake kufanya vizuri kwenye mashindano yote iliyoshiriki ingawa haikuweza kubeba taji lolote kati ya hayo.

Uwezo wa Dante, ulionekana zaid pale alipofanikiwa kumdhibiti mshambuliaji wa Young Africans Donald Ngoma asipeleke madhara kwa kipa wake Said Mohamed katika mchezo wa marudiano wa ligi, ingawa mchezo huo Young Africans walishinda kwa bao 1-0.

 1. Pascal Wawa

Beki mahiri mwenye uwezo mkubwa anayeichezea klabu ya Azam FC, ameingia kwenye kikosi hiki kutokana na uwezo aliokuwa nao na mchango wake kwa Azam haina ubishi uwepo wa Wawa kuna ongeza hata uimara wa kipa Aishi Manula.

Mlinzi huyu wa kati kutoka Ivory Coast, amekuwa akicheza kwa kujitoa na kusaidia sana mafanikio ya timu hiyo kwa msimu mmoja na nusu ambao tayari ameichezea timu hiyo na ukitaka kuona kama anamchango mkubwa kwenye timu hiyo angalia pale alipoumia  na kukosa mechi za mwishoni mwa msimu huu timu hiyo haikuwa na mwenendo mzuri kiasi cha kupoteza hata mbio za ubingwa na kufungwa mabao 3-1 na Young Africans kwenye mchezo wa fainali wa Kombe la FA.

 1. Jean Baptiste Mugiraneza

Huyu ni kiungo Mnyarwanda anayeichezea klabu ya Azam amekuwa akifanya kazi kubwa kuipigania timu yake hiyi tangu alipojiunga nayo mwanzoni mwa msimu akitokea APR.

Akiwa katika msimu wake wa kwanza tayari ameonyesha kama yeye  ni hodari kwa kuweza kuimudu vyema nafasi ya kiungo mkabaji na kuwaweka benchi wachezaji Frank Domayo na Michael Bolou ambao walikuwa wakijinafasi hapa awali kabla ya ujio wake.

 1. Farid Mussa

Winga hatari kabisa ambaye kiwango alichokionyesha msimu huu hakina mpinzani na kinamfanya kuingia kwenye kikosi bora cha msimu huu pasipo kupigwa kutokana na mchango alioutoa kwa timu yake ya Azam lakini pia timu ya taifa.

Mussa analazimika kumshukuru kocha Stewart Hall wa Azam ambaye alichangia kupandisha kiwango chake na hivi karibuni mchezaji huyo huenda akajiunga na timu ya Tenerife Deportivo inayoshiriki ligi daraja la kwanza nchini Hispania baada ya kufuzu majaribio aliyofanya kwa wiki tatu .

 1. Thabani Kamusoko

Tangu atue kwenye kikosi cha Young Africans msimu huu bado hajaonekana mchezaji mwingine wa nafasi ya kiungo mchezeshaji atakaye weza kumuondoa kwenye nafasi hiyo  Mzimbabwe huyo ambaye ameonyesha uwezo mkubwa wa kutoa pasi na kuichezesha timu lakini hata kufunga.

Kiwango kilichoonyeshwa na Kamusoko kinamfanya  kumuweka pembeni Haruna Niyonzima na kuchukua nafasi hiyo kutokana na umahiri wake wa ukabaji kuisaidia safu ya ulinzi kupunguza presha ya mashambulizi.

 1. Amissi Tambwe

Idadi ya mabao 21 aliyoifungia Young Africans msimu huu ni wazi anastaili kuwa kwenye kikos cha wachezaji 11 bora waliofanya vizuri msimu huu uliomalizika siku za karibuni.

Tambwe amekuwa akipondwa kuwa ni mchezaji wa kawaida lakini amekuwa na madhara makubwa anapokuwa kwenye lango la timu pinzani uwezo wake wa kufunga kwa kutumia kichwa na miguu umemfanya kuibuka mfungaji bora kwa mara ya pili akiwa na timu za Simba na Young Africans.

 1. Donald Ngoma

Hapana shaka kiwango kilichoonyeshwa na Donald Ngoma kimekata kiu ya mashabiki wa timu hiyo kuiona timu yao ikiwa na mtu ambaye inaweza kujivunia kama wapinzani wao Simba walivyokuwa wakijitambia walipokuwa na Emmanuel Okwi.

Sifa kubwa aliyoiweka Ngoma msimu huu nu kuzifunga timu zote kubwa kubwa Azam, Simba, Mtibwa Al Ahly na APR, huku akionyesha uwezo mkubwa wa kupambana na kumaliza nafasi ya tatu kwa ufungaji bora sifa hizo zinamfanya Mzimbabwe huyo kuingia kwenye kikosi hicho na kutokana na uwezo aliokuwa nao.

 1. Shizza Kichuya

Winga hatari wa Mtibwa Sugar amekuwa na msimu mzuri kiasi cha kumshawishi kocha wa timu ya taifa ya bTanzania Boniface Mkwassa kumjumuisha kwenye kikosi chake kitakachovaana na Misri Jumamosi hii.

Kichuya ameingia kwenye kikosi hiki bora msimu huu kutokana na cnhango alioutoa kwa timu yake ya Mtibwa kwenye mashindano yote waliyoshiriki msimu huu ikiwemo michuano ya Kombe la mapinduzi ambapo walifungwa na URA ya Uganda kwenye mchezo wa fainali.

Polisi yamng’ang’ania Mbowe Shinyanga
Video: Posho Yawapitia Mbali Wabunge Waliotoka Nje ya Ukumbi wa Bunge