Uwezekano wa Uingereza kujiondoa katika Umoja wa Ulaya bila ya mkataba umeongezeka kwa kiwango kikubwa kwa sababu mazungumzo juu ya suala hilo yanatishiwa na msimamo wa Uingereza wa kushikilia kwamba inayo mamlaka kamili juu ya mipango ya misaada inayotolewa na serikali.
Mwanadiplomasia wa ngazi ya juu kwenye Umoja wa Ulaya amesema hofu inaongezeka, nchini Uingereza, kwenye Umoja wa Ulaya na katika nchi nyingine na kwamba bila ya mkataba wa biashara kufikiwa,vurugu zaidi za kiuchumi zitafuatia katika muktadha wa janga la corona ambalo limeathiri uchumi wa nchi za Ulaya.
Amesema masoko ya fedha yataathirika vibaya na kusababisha hasara ya karibu dola trilioni moja katika sekta za magari, madawa, kilimo na uvuvi.
Waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson amesema nchi yake iko tayari kwa matokeo yoyote. Hata hivyo rais wa baraza la Umoja wa Ulaya Charles Michel ameitaka Uingereza ifafanue juu ya inachokitaka.