Serikali imewasilisha Bungeni Miswada ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali ya mwaka 2016, mojawapo ikiwa kuanzishwa kwa mahakama ya Mafisadi, wala rushwa na wahujumu uchumi iliyotoa picha ya hukumu itakayotolewa.

Kwa mujibu wa Muswada huo, marekebisho ya sheria yaliyowasilishwa yatapelekea kuanzishwa kwa Divisheni ya Mahakama Kuu ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi itakayokuwa na mamlaka ya kusikiliza na kuamua kesi hizo.

Muswada huo umeeleza wazi watakaokutwa na hatia ya makosa hayo katika Mahakama hiyo maalum itakayoanzishwa watahukumiwa kifungo kisichopungua miaka 20 jela na kisichozidi miaka 30.

Unzishwaji wa Divisheni ya Rushwa na Uhujumu uchumi katika Mahakama Kuu ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi ya Rais John Magufuli aliyoitoa wakati wa kampeni za uchaguzi Mkuu. Alisema ataanzisha Mahakama hiyo katika jitihada za kupambana na rushwa na ufisadi ili hukumu zitolewe mapema kwa watu wenye makosa hayo.

Muswada huo ukipitishwa na Bunge, utasubiri saini ya Rais John Magufuli kuwa Sheria huku Kanuni zake zikiandaliwa na ofisi ya Jaji Mkuu.

“Taratibu nyingine za uendeshaji na utekelezaji wa masharti ya sheria hii itakuwa katika kanuni zitakazoandalaiwa na Jaji Mkuu,” umeeleza Muswada huo.

Kikwete: Ni jukumu la Ulaya kuipa Afrika Misaada, Hatuwezi Kuikwepa
ukataji wa miti kukoma!!