Hukumu ya kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya na wenzake sita imeahirishwa hadi Juni 10, 2022.
Kesi hiyo imeahirishwa hii leo Mei 31, 2022 na Hakimu mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu mkazi Arusha Fadhil Mbelwa kutokana na Hakimu anayeisikiliza kesi hiyo kuwa na majukumu mengine.
“Shauri hili lipo kwa Hakimu mkazi Mwandamizi Patricia Kisinda lakini leo amepangiwa majukumu mengine nje ya ofisi na hataweza kutoa hukumu hadi Juni 10, 2022,” amefafanua Mbelwa.
Mbali na Sabaya watuhumiwa wengine katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 27/2021 ni Nyegu, Jackson, Watson Mwahomange, Nathan Msuya, Enock Mnkeni, John Aweyo na Sylvester Macha.
Upande wa utetezi wa washitakiwa sita umewakilishwa na Mawakili Sylvester Kahunduka, Fridolin Bwemelo, Mosses Mahuna na Edmund Ngemela huku mtuhumiwa mmoja Watson Mwahomange akijitetea mwenyewe.
Aidha Jamhuri imewakilishwa na Mwendesha mashitaka wa Taasisi ya kupambana na kuzuia rushwa nchini (TAKUKURU), Jacopiyo Richard, Mawakili wa Serikali waandamizi Janeth Sekule, Felix Kwetukia na Neema Mbwana.
Mei 6, 2022 Mahakama Kuu ya Tanzania ilitoa uamuzi wa kushinda kwa rufaa iliyokatwa na Sabaya na wenzake katika jitihada za kubatilisha hukumu iliyotolewa ya kifungo cha miaka 30 kutokana na makosa matatu ikiwemo Unyang’anyi wa kutumia silaha.
Hata hivyo licha ya kushinda rufaa hiyo Sabaya alibaki mahabusu akiendelea na kesi nyingine inayomkabili ya uhujumu uchumi ambayo haina dhamana kwa mujibu wa sheria za nchi.
Sabaya ni miongoni mwa wanasiasa vijana waliokuwa na nguvu wakati wa utawala wa Hayati John Magufuli akiwa Mkuu wa Wilaya ya Hai akitokea kwenye nafasi ya mwenyekiti wa vijana Umoja wa vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Arusha aliyokuwa akitumikia.