Ndoto za klabu ya Man Utd za kutaka kumsajili beki wa kati wa klabu ya Borussia Dortmund, Mats Hummels, zimeyeyuka baada ya mambo kwenda tofauti.

Hummels, kwa mara ya kwanza amezungumzia sakata lake la kuondoka nchini Ujerumani na kwenda kusaka mkate wake wa kila siku mahala pengine na ambapo amesema kuwa haoni sababu ya kufanya hivyo katika kipindi hiki.

Beki huyo mwenye umri wa miaka 26, amesema mambo mengi yamezungumzwa dhidi yake na wakati mwingine alikuwa akikasirishwa na kile kilichokuwa kikivumishwa, lakini maamuzi yake ya mwisho ni kuendelea kusalia Signal Iduna Park kwa mwaka mmoja zaidi.

Amesema anauheshimu sana mkataba alionao kwa sasa, na litakuwa jambo la kipuuzi kama atakwenda kinyume na uongozi huo ambao unampa ruhusa ya kuendelea kuwa sehemu ya kikosi cha BVB.

Hummels, amesaliwa na mkataba wa miaka miwili na kwa maelezo aliyoyatoa atakuwa tayari kuondoka nchini Ujerumani ama kuhamia kwenye klabu nyingine nchini humo mara baada ya msimu wa 2015-16.

Hummels, alijiunga na Borussia Dortmund, mwaka 2009 kwa mkataba wa mkopo akitokea kwa mabingwa wa soka nchini Ujerumani, FC Bayern Munich na baada ya hapo alisajiliwa moja kwa moja.

Van Persie Aendelea Kuandamwa Na Jinamizi Hili
Djokovic Atishia Mazingira Ya Ubingwa Wimbledon Open