Mwenyekiti wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Murtaza Mangungu amesema wamejipanga kuvuna alama sita za michezo miwili ya mwisho ya Duru La Kwanza la Ligi Kuu Tanzania Bara.
Simba SC leo Alhamis (Februari 03) itacheza dhidi ya Tanzania Prisons Uwanja wa Benjamin Mkapa saa moja usiku, huku ikitarajia kumaliza Duru La Kwanza Jumapili (Februari 06) kwa kucheza dhidi ya Mbeya Kwanza FC.
Mangungu amesema lengo kubwa la Simba SC katika michezo hiyo miwili ni kuhakikisha inapata alama zote sita ambazo zitawasaidia katika mpango mkakati wa kutetea ubingwa wao Msimu huu 2021/22.
Amesema baada ya michezo ya Duru La Kwanza kukamilika, Simba SC imejipanga kuanza Duru La Pili kwa nguvu zote huku ikiwa makini kwa kutorudia makosa walioyafanya kwenye michezo kadhaa na kupoteza alama 10, ambazo zinaleta tofauti kati yao na Young Africans inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu kwa sasa.
“Tumebakiza michezo miwili kabla ya kumaliza mechi za mzunguko wa kwanza. Tumejipanga kupata alama zote sita kwenye michezo hiyo na kuanza mzunguko wa pili kwa nguvu mpya.” Amesema Mangungu
Baada ya mchezo dhidi ya Mbeya Kwanza FC siku ya Jumapili (Februari 06), Simba SC itaanza kujiandaa na Mshike Mshike wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika hatua ya Makundi, ambapo itaanzia nyumbani Februari 13 kwa kucheza dhidi ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast.
Baada ya hapo Simba SC itasafiri kwenda ugenini wakiifuata Union Sportive Gendarmerie Nationale (USGN) ya Niger katika mchezo wa pili wa hatua ya Makundi kisha kurejea tena nyumbani kuikaribisha Biashara United Mara katika mchezo wa Mzunguuko wa 16 wa Ligi Kuu ambao utakua wa kwanza kwa Duru la Pili la Ligi hiyo.