Mwanzoni mwa juma hili Uongozi wa Azam FC ulithibitisha kumuajiri Kocha Youssouph Dabo raia wa Senegal akichukua nafasi ya Kally Ongala aliyekuwa akikaimu nafasi ya kuliongoza Benchi la Ufundi la Klabu hiyo.
Dabo ametua kwenye timu hiyo baada ya kuachana na ASC Jaraaf de Dakar huku akikumbukwa zaidi baada ya kuifundisha Teungueth iliyokuwa na staa wa Simba SC, Pape Sakho na Malikcou Ndoye wa Azam FC.
Desemba 2019, Dabo aliiongoza Senegal kushinda ubingwa wa Kanda ya Wafu mashindano yaliyofanyika Guinea na Machi 2020 aliiongoza Senegal kushinda ubingwa wa vijana chini ya miaka 20 katika mashindano ya mataifa ya Kiarabu ikishiriki kama wageni waalikwa yaliyofanyika Saudi Arabia.
Novemba 2020, akiwa kocha wa timu ya taifa ya Senegal chini ya miaka 20 alifika fainali kuwania ubingwa wa kanda A ya Afrika Magharibi na msimu wa 2020/21 alishinda ubingwa wa Ligi ya Senegal akiwa na Teungueth.
Msimu wa 2020/21, Dabo akiwa na Teungueth iliiwezesha timu hiyo kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuishangaza Raja Casablanca ya Morocco kwenye mchezo wa raundi ya kwanza.
Mchezo wa kwanza uliofanyika Senegal ulimalizika kwa 0-0 sawa na mechi ya marudiano iliyopigwa pale nchini Casablanca kisha kuamuliwa kwa mikwaju ya penalti ndipo Teungueth ikashinda 3-1.
Kuajiriwa kwa Dabo hakuwezi kuathiri nafasi ya Ongala kwani huenda akarejea nafasi yake ya mwanzo aliyokuwa anaitumikia ya kuendelea kuwa kocha wa washambuliaji ndani ya kikosi hicho.
Kally alipewa kibarua hicho baada ya Klabu hiyo kuachana na aliyekuwa Kocha Mkuu Mfaransa, Denis Lavagne aliyetimuliwa Oktoba 22 mwaka jana kutokana na matokeo mabovu yaliyokuwa yanaiandama.