Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima ametoa wito kwa wananchi wote kujenga tabia ya kuwasikiliza Wataalamu wa Afya ili kuishinda vita dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.

Dkt. Gwajima amesema hayo leo Agosti 11, 2021 wakati akifungua Mkutano wa Wataalamu wa masuala ya Afya wenye lengo la kujadili njia bora ya kupambana dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza, uliofanyika katika ukumbi wa chuo cha Muhimbili (MUHAS) Jijini Dar es Salaam.

“Wito wangu kwa wananchi kuhusiana na magonjwa yasiyoambukiza ni tuwasilikilize Wataalamu wa Afya, Wataalamu wa Afya siku zote wana lengo la kuelimisha ili wananchi wapate elimu na maamuzi sahihi kwenye Afya zao,” Amesema Dkt. Gwajima .

Dkt. Gwajima amesema kuwa yapo magonjwa yasiyoambukiza ambayo mtu anazaliwa nayo lakini pia yapo ambayo yanasababishwa na mtindo wa maisha ya wananchi wenyewe kama vile ulaji usiofaa, matumizi ya vilevi kupita kiasi, matumizi ya vyakula vya mafuta mengi, uvutaji sigara na kutofanya mazoezi.

Amesema, ulaji usiofaa ambao unapelekea viliba tumbo na utapiamlo ni moja ya visababishi vya magonjwa yasiyoambukiza nchini, licha ya nchi ya Tanzania kubalikiwa kuwa na mikoa inayolima aina zote za mazao ya vyakula.

Kwa upande mwingine amesema, Serikali ilishatoa agizo kwa wanaofanya biashara zinazozalisha kelele na kusababisha magonjwa na usumbufu kwa wananchi ni lazima wafuate maelekezo yaliyotolewa na Serikali ikiwemo kuzuia kelele hizo zisiende kwa wananchi kwa kiwango kikubwa.

Aidha, Dkt. Gwajima amesema kuwa, Serikali kupitia Sekta zake imejipanga kushirikiana kwa kuja na Sera na mikakati mizuri itayosaidia wananchi katika mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza, huku akiwataka wananchi kufuata maelekezo ya Serikali ili kuondokana na magonjwa haya.

Hata hivyo, Dkt. Gwajima amesema kuwa, Wizara ya Afya kupitia Kurugenzi ya tiba asili na Baraza la tiba asili na tiba mbadala inaratibu bidhaa za tiba asili zote nchini, ikiwemo bidhaa zitazosaidia kutibu magonjwa yasiyoambukiza ili kulinda Afya za wananchi.

Gazeti la Uhuru lafungiwa
Rais Samia afanya mazungumzo na TLS ,TAWJA