Spika wa Bunge, Job Ndugai, amesema kuwa Mbunge wa Shinyanga Mjini kupitia chama cha mapinduzi (CCM), Steven Masele hawezi kukaidi tena agizo la kutakiwa kufika katika Kamati ya Maadili baada ya kuitwa na Spika huyo kwa mara ya pili.
Ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo, Ndugai amesema kuwa suala la Bunge kumuita Masele halihusiani na matukio yaliyotokea Afrika Kusini bali ni kwa sababu ya mambo aliyofanya nyumbani.
Ameitwa kwa mambo ya hapa nyumbani ya utovu wa nidhamu, anaunganisha hilo na matendo anayoyafanya huko, lakini hatujamuita kwa mambo ya South Afrika Watanzania watulie baada ya muda zitaletwa bungeni kila mtu atasikia kuhusu anatuhumiwa nini na majibu yake yalikuwa nini na wataelewa kama ameonewa au hajaonewa. Steven Masele hawezi kukaidi zaidi kwa sababu ni lazima arudi Tanzania, labda sababu awe mkimbizi na akirudi Tanzania lazima aje Kamati ya Maadili, ni wito wa kisheria tunachomuitia ni tabia yake uchonganishi wa viongozi, kwa sasa hatuwezi kusema ila akishatoka mtaelewa fitina ikoje, ambayo ni kukosa sifa kwa kiongozi yeyote yule”, amesema Spika Ndugai.
Kwa mujibu Masele amesema kuwa kwasasa yuko njiani kuja Tanzania kwa ajili ya kuitikia wito wa Spika Ndugai ikiwa ni siku chache baada ya kumaliza sakata la kupokea ripoti inayomuhumusu Rais wa Bunge la Afrika, Roger Nkodo Dang iliyokuwa ikimuandama.