Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Bashiru Ally amesema kuwa Waziri wa Viwanda, Innocent Bashungwa atatumbuliwa ikiwa atashindwa kutimiza azma ya Serikali ya kufufua viwanda.
Ameyasema hayo baada ya kutembelea kiwanda cha kukoboa kahawa cha TCCCO kilichopo Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro.
Amesema kuwa ajenda ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kufufua viwanda na kwamba jambo linalopaswa kufanya ni kujiandaa katika masuala ya ushirika, ubunifu na ujuzi ili nchi iweze kujisimamia.
“Nimesoma katika kitabu cha wageni waziri wa Viwanda alikuwa hapa Mei 28 (aliyekuwa Waziri wa Viwanda, Joseph Kakunda) na ameshatumbuliwa, na huyu aliyepo ajiandae kutumbuliwa maana kama tunasema tunahitaji uchumi wa viwanda halafu havifufuki, wakati mnaona kabisa barabara zinajengwa unaziona, SGR (Reli ya kisasa) unaiona, kwa nini hatuoni viwanda vinafufuliwa?”amehoji Dkt. Bashiru.
Aidha, amesema kuwa kuendesha kiwanda kama TCCCO ni lazima kuwepo na kiwanda cha magunia, ambapo bado kuna kazi kubwa katika vita ya uchumi kiwanda hicho ambacho kilitarajiwa kuwa na wafanyakazi zaidi ya 4000 lakini mpaka sasa kina wafanyakazi 44 tu, mitambo inaitwa mipya lakini haifanyi kazi na imenunuliwa kwa kuuza mali za kampuni, ambapo ameziita kuwa hizo ni hujuma.
Amebainisha kuwa viwanda vyote vilivyoanzishwa wakati wa Serikali ya Awamu ya Kwanza vina hali mbaya hivyo amemtaka waziri husika kufanya jitihada ya kuvifufua viwanda hivyo.
Kwa upande wake makamu mwenyekiti wa bodi ya kiwanda hicho, TCCCO, Kandata Kimaro amesema kuwa kiwanda kinadaiwa Sh1.2 bilioni na kwamba Kahawa inayopokewa kiwandani imeshuka kutoka tani 31,000 mwaka 1988/1989 hadi tani 912 msimu wa mwaka 2018/2019.