Ibada maalum kwa ajili ya kumuombea aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli imefanyika katika Kanisa Katoliki la Mt. Yohana Maria Muzeyi, la Parokia ya Mlimani, lililopo Chato Mkoani Geita.
Ibada hiyo imefanyika hii leo Machi 17, 2023 ikiwa imepita miaka miwili na ni siku ambayo alifariki Dkt. John Magufuli ambayo imeongozwa na Askofu Mkuu Jimbo la Katoliki la Rulenge – Ngara, Severine Niwemugizi.
Aidha, katika ibada hiyo pia ilihudhuriwa na Viongozi na watu mbalimbali wakiwemo na waumini, huku mjane wa Hayati Magufuli, Janeth Magufuli akiwaongoza wanafamilia Kanisani hapo ambapo Askofu Niwemugizi amesisitiza juu ya somo la upendo na mshikamano wa Watanzania.
Dkt. Magufuli alifariki dunia Machi 17, 2021 katika hospitali ya Mzena mkoani Dar es Salaam na kuzikwa katika Kijiji cha Mlimani Wilayani Chato Mkoa wa Geita, katika makaburi ya familia ambapo majonzi, simanzi na huzuni vilitawala makaburini, wakati mwili wake ukishushwa kaburini.