Mlinda Lango wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Aishi Manula, ameendelea kumnyima usingizi aliyekua Kocha Mkuu wa AS Vita Club ya DR Congo Florent Ibenge.
Ibenge ambaye kwa sasa ni Kocha wa RS Berkane ya Morocco, amesema Mlinda Lango huyo wa Tanzania amekua chachu kubwa kwa ubora wa kikosi cha Simba ambacho msimu uliopita kilifika Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Amesema tangu msimu uliopita katika michuano hiyo, Simba SC ndio timu yenye safu bora ya ulinzi lakini ubora wa safu hiyo, unachagizwa na uimara Aishi Manula
“Nafikiri tangu msimu uliopita Simba SC ndio klabu yenye safu bora ya ulinzi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, na ubora huo unachagizwa sana na Mlinda Lango wao Aishi Manula.”
“Kwa sasa huyu Manula ni mmoja wa Walinda Lango Bora wanaocheza hapa Afrika, nampongeza kwa kweli, pia naipongeza Simba SC kwa kuwa na mtu kama huyu.” amesema Ibenge
Kwa msimu huu 2021/22 Aishi Manula ameanza vyema michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, baada ya kutoruhusu bao katika mchezo wa jana Jumapili (Oktoba 17) dhidi ya Jwaneng Galaxy, uliomalizika kwa Simba SC kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 mjini Gaborone, Bostwana.