Afisa Mtandaji Mkuu wa Simba SC Imani Kajura ameweka sawa suala la Mshambuliaji kutoka DR Congo Jean Othos Baleke, ambaye amekuwa gumzo katika kipindi hiki, kufuatia kuibeba timu hiyo katika Michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara na Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Kufanya vizuri kwa Baleke, kumeibua sintofahamu ya mustakabali wake ndani ya Simba SC, ambapo baadhi ya wadau wamekuwa wakidai Mshambuliaji huyo ataondoka mwishoni mwa msimu huu kufuatia mkataba wa mkopo aliousaini Mwezi Januari mwaka huu, lakini Uongozi wa klabu umesisistiza ana mkataba wa miaka miwili.
Kajula amesema ni kweli Baleke yupo Simba SC kwa mkopo wa muda mrefu, lakini Uongozi unaangalia uwezekano wa kuendelea kuwa naye klabuni hapo kwa kumsainisha mkataba wa jumla.
Kiongozi huyo amesema Beleke amekuwa na mazingira mazuri tangu alipojiunga na Simba SC kwa mkopo akitokea TP Mazembe ya nchini kwao DR Congo, hali ambayo inamfanya kuishi kwa furaha na kutimiza wajibu wake kwa vitendo uwanjani.
“Baleke ana furaha kuwa Simba, ana shauku ya kufanya makubwa akiwa na timu hiyo na kwa sasa hana malengo ya kuondoka hivyo mashabiki wake wasiwaze juu ya hilo.”
Katika hatua nyingine Kajula amesema kuwa, hakuna mchezaji ambaye Simba SC inamuhitaji atakayeondoka na zaidi watafanya maboresho ya mikataba yao.
“Hakuna mchezaji ambaye ataondoka Simba SC kama bado huduma yake inahitajika, tutakacho kifanya ni kuboresha baadhi ya mikataba ambayo inakaribia mwisho na mingine kutokana na makubaliano ya pande zote mbili yalivyo.” amesema Kajula
Taarifa zinaeleza kuwa Mabigwa wa Soka nchini Sudan Al Hilal wakiongozwa na Kocha Mkuu Florent Ibenge wamedhamiria kumsajili Baleke kwa kununua sehemu ya mkataba wake na TP Mazembe.
Thomas Partey aivimbia Manchester City
Ibenge ambaye ni raia wa DR Congo anaamini Mshambuliaji huyo atakuwa na wakati mzuri zaidi endapo atafanikiwa kumsajili mwishoni mwa msimu huu, licha ya kubainika wazi Baleke amesaini Mkataba wa Mkopo wa miaka miwili Simba SC.
Baleke ana mkataba wa miaka mitano na TP Mazembe, lakini tayari ameshatumika kwa mwaka mmoja, na miaka miwili atacheza Simba SC, hivyo atasaliwa na mwaka mmoja atakapomalizana na Mnyama msimu wa 2024/25.