Kocha Mkuu wa AS Vita Club Florent Ibenge ametamba kuifunga Simba SC kwenye mchezo wa mzunguuko wa tano wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika hatua ya Makundi, utakaochezwa kesho Jumamosi (April 03), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Ibenge ametamba kufanya hivyo, baada ya kuwasili Dar es salaam sanjari na kkosi chake jana Alhamis (April Mosi), wakitokea mjini Kinshasa, DR Congo tayari kwa mchezo huo ambao utahudhuriwa na mashabiki 10,000.

Kocha huyo ambaye pia ni mkuu wa benchi la ufundi la timu ya taifa ya DR Congo amesema, amekiandaa kikosi chake ipasavyo ili kufanikisha lengo la kuibuka na ushindi dhidi ya Simba SC ambayo itakua nyumbani.

Hata hivyo kocha huyo amekiri kuwa, licha ya kujiwekea mipango ya kushinda ugenini, bado anaamini mchezo wa kesho utakua mgumu kutokana uimara wa wenyeji wao (Simba SC), ambao hawajawahi kupoteza mchezo wa kimataifa nyumbani tangu mwaka 2012.

“Tumekuja kucheza, ni mechi ngumu ambayo tutahitaji matokeo chanya ili kujiweka mahali salama kuelekea hatua inayofuata. Nadhani dakika 90 za mchezo huo zitakuwa nzuri na zenye ushindani mkubwa,” amesema Ibenge.

Mchezo huo ni wa marudiano katika hatua ya Makundi ambapo utazikutanisha timu hizo mbili kutoka ‘KUNDI A’ baada ya mchezo wa kwanza uliopigwa Kinshasa-DR Congo, Simba kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

Katika mchezo huo Simba mwenye alama 10 kileleni mwa ‘KUNDI A’ ikifuatiwa na Al Ahly wenye alama saba, watahitaji matokeo ya sare au ushindi ili kufuzu hatua inayofuata ya robo fainali huku AS Vita aliye nafasi ya tatu na alama nne atahitaji ushindi ili kufufua matumaini ya kusonga mbele.

Mchezo wa mwisho hatua ya makundi Simba itacheza na Al Ahly ugenini huku AS Vita watawakaribisha Al Merrikh nyumbani kwao Kinshasa.

BAKITA wafunguka Hayati Magufuli alivyokipaisha Kiswahili
Madareva 10 wa mabasi wafungiwa kwa mwendokasi