Kiungo Mshambuliaji wa Singida Fountain Gate FC, Ibrahim Ajibu, ameendelea kuimarika kutokana na majeraha aliyokuwa nayo hali iliyompelekea kukaa nje kipindi cha miezi mitatu.
Akizungumza jijini Dar es salaam, Ajibu amesema kwa sasa anaendelea vyema na tayari ameanza kufanya mazoezi mepesi.
“Ninashukuru hali yangu inaendelea vizuri baada ya kukaa nje muda mrefu ninaamini msimu ujao nitakuwa nimeimarika zaidi, amesema Ajibu
Amesema maendeleo yake ya sasa yanampa matumaini ya kuanza mazoezi mapema ya kujiweka sawa kuelekea kwenye msimu ujao ambao ameahidi kufanya vizuri zaidi.
Mshambuliaji huyo amesema alishindwa kuonyesha makali yake msimu uliopita kufuatia majeraha hayo na kuahidi kuendeleza kiwango chake.
“Nitarudi tu kwenye kiwango changu, kikubwa ilikuwa kupona kwanza, nashukuru Mungu hali yangu ya sasa, nimeanza mazoezi mepesi na ndani ya muda mfupi nitarejea kwenye mazoezi ya nguvu kabla ya kuanza maandalizi na timu yangu kuelekea kwenye msimu mpya,” amesema Ajibu
Ajibu alijiunga na Singida Big Stars (Sasa Singida Fountain Gate) msimu uliopita akitokea Azam FC ambapo hakupata nafasi kubwa ya kucheza.