Baada ya kuondoka Azam FC, Kiungo Mshambuliaji Ibrahim Ajib kwa mara ya kwanza amefungua kinywa chake na kueleza matarajio aliojiwekea, katika sehemu ya msimu wa 2022/23 iliyosalia.
Mwanzoni mwa juma hili Azam FC ilitbibitisha kuachana na Kiungo huyo wa zamani wa klabu za Simba SC na Young Africans zote za Dar es salaam, na kumtakia kila la kheri katika makazi yake mapya kisoka.
Ajibu amesema kwa sasa anaendelea kujiandaa vizuri huku akimuomba Mwenyezi Mungu amjaalie afya njema, ili kufanikisha mpango aliojiwekea, baada ya kuondoka Azam FC.
Amesema kuondoka kwake Chamazi kunachukuliwa kama ameshindwa kuonesha uwezo wa kisoka, jambo ambalo amesema sio kweli na badala yake ameahidi kuwafunga midomo waliozusha taarifa hizo.
“Namuomba Mungu anipe afya njema nataka kwenda kuonyesha mfano, siyo kama nilishindwa kucheza Azam FC kwa ajili ubora, binafsi sipendi kuongea bali nitakwenda kuonyesha vitendo,” alisema Ajibu na kuongeza;
“Maisha yangu kwa kiasi kikubwa yapo kwenye mpira nikuhakikishie kila ninalolifanya ni sahihi kwa hatma yangu kwa sasa na hapo baadaye nitakapoachana na Soka.”
“Kutokana na usajili wangu mpya ulivyo kuna kazi kubwa natakiwa kwenda kuifanya kwenye timu yangu mpya binafsi naamini hilo linawezekana kwa kushirikiana na wachezaji wenzangu,” amesema Ajibu
Mbali na Kimya kilichotawala huku tetesi za mitandao zikichukua nafasi kubwa kuwa Ibrahim Ajibu amesajiliwa Singida Big Stars, bado Uongozi wa Klabu hiyo ya mjini Singida haujathibitisha usajili wa mchezaji huyo ambaye pia amewahi kuitwa kwenye Timu ya Taifa Tanzania ‘Taifa Stars’.