Kiwango kilichooneshwa na Beki wa Klabu ya Young Africans Ibrahim Abdallah ‘Bacca’ wakati wa mchezo wa kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ dhidi ya Uganda, kimemkosha mfadhili wa zamani wa klabu ya Simba SC Azim Dewji.
Bacca alicheza kwa mara ya kwanza katika kikosi kilichoanza cha Stars kwenye mchezo huo ambao ulishuhudia Stars ikichomoza na ushindi wa 0-1, ikicheza ugenini nchini Misri.
Azim Dewji aliyewahi kuipa Simba rekodi tamu alipoifadhili klabu hiyo miaka ya 1990 akiifikisha Fainali za Kombe la CAF 1993 na kupoteza kwa Stella Abidjan, amesema beki huyo wa Young Africans alionesha soka safi na kuisaidia Stars kuwa salama wakati wote.
Dewji amesema Young Africans imemkosha kwa skauti iliyomuibua Bacca aliyeonyesha kiwango bora kwa timu hiyo na kuibeba Stars, ambayo inaendelea na mchakato wa kusaka nafasi ya kushiriki Fainali za AFCON 2023.
“Niwapongeze sana Young Africans kwa skauti yao ni bora, hakuna aliyemjua Bacca, binafsi nilimuona walivyocheza na Watunisia (US Monastir),”
“Nikamuona tena akiwa na Stars ni beki bora hadi nikajiuliza Young Africans imemtoa wapi? nikaambiwa aliibukia Pemba kisha akaenda Unguja ndio Young Africans wakamsajili wakati wa Dirisha Dogo la msimu uliopita akitokea KMKM, Hili linathibitisha Tanzania tuna vipaji vizuri kama tutakuwa na akili ya kuviendeleza namna hii, beki huyu analisaidia taifa.” amesema Dewji aliyewahi kuwa Kamati ya Saidia Stars ishinde miaka ya 1990 na kuiwezesha kutwaa Kombe la Chalenji 1994
Wakati huo huo Dewji amewataka mashabiki kujitokeza kwa wingi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kesho Jumanne (Machi 28) kuishangilia Taifa Stars wakati itakapoarudiana dhidi ya Uganda.