Bondia wa ngumi za kulipwa nchini Tanzania, Ibrahim Class amesema atamchapa mpinzani wake Xion Tau Su kutoka China, kwa KO katika pambano litakalofanyika kesho Jumamosi (Oktoba 28).

Mabondia hao, wanatarajiwa kupanda ulingoni kupigana raundi 10 uzito wa kati katika Ukumbi wa PTA, Sabasaba jijini Dar es Salaam.

lbrahim Class amesema amemaliza mazoezi na hivi sasa anasubiri muda ufike ashinde kwa KO.

“Nimejiandaa vizuri kupambana na mpinzani wangu kwa sababu nilikaa kambi ya Tanga chini ya kocha wangu Master Habibu Kinyogoli, “amesema lbrahim Class.

Naye Promota wa pambano hilo, Hamisi Kumbucha amesema baada ya kumaliza pambano hilo wanatarajia kuandaa mapambano mengine.

“Kwa mara kwanza Tanzania kunachezeka mkanda wa Ubingwa wa WBC Afrika, kupitia bondia, Fadhili Majiha ambaye atacheza na Bongani Mahlangu kutoka Afrika Kusini, “amesema.

“Pia, hali ya ulinzi itakuwa nzuri kwani tumejipanga vyema kuhakikisha pambano linapigwa huku hali ya usalama ikiwa katika mazingira mazuri,” amesema Kumbucha.

Kwa upande wa Bondia, Fadhili Majiha amewaomba Watanzania kujitokeza kwa wingi kushuhudia anavyompiga mpinzani wake, Bongani Mahlangu kutoka Afrika Kusini.

“Nimejipanga vizuri kushinda mchezo huo dhidi ya Mahlangu ndani ya raundi zote 12 na kubakisha mkanda nyumbani.

“Ninasema kamwe Mahlangu hawezi kutamba mbele yangu,” amesema.

Majiha anashuka ulingoni akiwa na kumbukumbu ya kumpiga Renz Rosia kutoka Ufilipino kwa kushinda mkanda wa UBO.

Kocha Liverpool athibitisha upasuaji wa Robertson
CCM ipo imara kutatua changamoto za Wananchi