Bondia wa ngumi za kulipwa nchini, Ibrahim Mgenda “Ibrahim Class’ ameingia kambini rasmi ili kujiandaa na pambano dhidi ya Xion Tau Su kutoka China litakalofanyika Oktoba 28, mwaka huu kwenye Ukumbi wa PST Sabasaba, Dar es salaam.
Ibrahim Class na Su watacheza pambano la raundi 10 lakini lisilo la ubingwa wakiwasindikiza Fadhili Majiha atakayepigana na Mahlangu kutoka Afrika Kusini ambao watawania mkanda wa WBC.
Ibrahim Class amesema anaendelea vyema na maandalizi yake kuelekea pambano hilo ambalo anatarajia litakuwa zuri na lenye ushindani kutokana na ubora wa mpinzani wake.
“Nimeingia kambini mapema kwa sababu ya uzito wa pambano ambalo naenda kucheza lakini pia mpinzani ninayekutana naye sio wa kumbeza natakiwa kujiandaa vizuri zaidi,” amesema Ibrahim Class.
Naye Mratibu wa matukio na habari wa Kampuni ya HB Sadc Boxing, Abdallah Neneko amesema taratibu zote muhimu zimekamilika na wanatarajia wadau wa ngumi watapata burudani safi.
Neneko ametaja mapambano mengine yatakayochezwa siku hiyo itakuwa ni kati ya bondia Nassib Ramadhani dhidi ya Zolisa Batyi kutoka Afrika Kusini wakati Spumoni Muki ataonyesha ubabe na Loveleen Thaakur wa India.
“Kupitia kampuni yetu Watanzania wategemee mapambano mazuri na watashuhudia mabondia wenye viwango wakija kupigana nchini,” amesema Neneko.