Beki wa Klabu ya Liverpool Ibrahima Konate, amekiri kwamba anafikiria kuhusu uwezekano wa kuichezea Klabu ya nyumbani ya Paris Saint-Germain, baadae katika maisha yake ya soka.
Konate alitumia miaka mitano katika akademi ya vijana ya Paris kabla ya kuhamia Sochaux, ambako alifanya kazi yake ya kwanza mwaka 2017 akiwa na umri wa miaka 16.
Baadae mwaka huo huo, alijiunga na RB Leipzig na kuimarisha mchezo wake kama mmoja wa mabeki wa kati vijana bora zaidi Barani Ulaya.
Katika majira ya joto ya 2021, Liverpool walimsajili kwa Pauni Milioni 36 kumpeleka Anfield.
Tangu wakati huo, amekua mmoja wa mabeki bora wa Ligi Kuu England, ingawa amekuwa akijitahidi kujiweka sawa na amekuwa akipambana na majeraha.
Katika kiwango cha kimataifa, Konate ameichezea Ufaransa mara 13 tangu alipocheza kwa mara ya kwanza mwaka 2022 na amekuwa kipenzi cha kocha Didier Deschamps.
Aliingia akitokea benchi katika mchezo wa fainali ya Kombe la Dunia mwaka jana dhidi ya Argentina ambapo walifungwa kwa mikwaju ya Penati.
Kama ilivyo kwa wachezaji wengi wa Ufaransa, Konate amekuwa akihusishwa na kurejea nchini kwao kuichezea PSG.
Akiwa kwenye majukumu ya kimataifa mwezi uliopita, aliulizwa ikiwa wachezaji kutoka Parc des Princes walikuwa wakimuuza kwa wazo la kuhama.
“Sitajibu kuhusu wanachofanya! Lakini hapana, ni kweli kwamba mimi ni Mparis, lakini niko Liverpool,” aliiambia RMC wakati huo baada ya sare ya bao 1-1 ya Liverpool kwenye Uwanja wa Luton Town Jumapili (Novemba 05), Konate aliulizwa na Canal Plus kama anawazia kucheza PSG siku moja.
“Kama nikisema hapana, nitakuwa nasema uongo, lakini ikiwa unauliza, ni moja ya malengo yangu? Sivyo,” alisema.