Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC), imemkuta na hatia aliyekuwa kiongozi wa kijeshi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Bosco Ntaganda kwa makosa ya mauaji, ubakaji na kuwatumikisha watoto kwa shughuli za kijeshi.
Mahakama hiyo iliyoko jijini The Hague, imeeleza kuwa Ntaganda mwenye umri wa miaka 45 alifanya makosa hayo alipokuwa mkuu wa shughuli za kijeshi Mashariki mwa DRC tangu mwaka 2002 hadi 2003.
“Mahakama… baada ya kusikiliza maelezo yaliyotolewa na pande zote, imekukuta na hatia katika makosa ya mauaji ambayo ni kinyume cha haki za binadamu,” alisema Jaji Robert Fremr alipokuwa anasoma muhtasari wa hukumu, kwa mujibu wa Reuters.
Uamuzi huo ni ushindi wa nadra wa upande wa muendesha mashtaka katika mahakama hiyo iliyoanzishwa rasmi mwaka 2002 kwa lengo la kuendesha kesi za uvunjaji wa haki za binadamu na makosa ya kivita.
Mahakama hiyo imeeleza kuwa imemkuta Ntaganda na hatia katika makosa 18 kati ya yale yaliyowasilishwa.
Hata hivyo, wanasheria wa Ntaganda wameeleza kuwa mteja wao hajaridhika na uamuzi huo kwani waliovunja sheria za kijeshi ni wanajeshi aliokuwa amewapa amri wao wakatekeleza tofauti.
Hivyo, waliitaka Mahakama kuamuru kuwa waliotenda makosa hayo wakamatwe wao binafsi na kushtakiwa.
Ntaganda ambaye hakuonesha kuwa na wasiwasi wakati hukumu hiyo ilipokuwa ikisomwa amepewa siku 30 za kukata rufaa.