Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) iliyoko The Hague nchini Uholanzi, imemuachia huru aliyekuwa Rais wa Ivory Coast Laurent Gbagbo.
Gbagbo alikuwa anakabiliwa na mashtaka ya uhalifu dhidi ya binadamu kutokana na mauaji ya watu 3,000 yaliyotokana na vurugu zilizotokea mwaka 2010 nchini kwake baada ya kukataa kuachia madaraka licha ya kushindwa katika uchaguzi.
Mwanasiasa huyo alikamatwa na vikosi vya majeshi ya Umoja wa Mataifa pamoja na vikosi vya Ufaransa vilivyokuwa vinamuunga mkono mpinzani wake, Alassane Ouattara.
Vurugu hizo zilizodumu kwa takribani miezi mitano zilisababisha mauaji ya kutisha kuwahi kutokea nchini humo.
Mauaji yalishuhudiwa zaidi katika maeneo ya mji wa Abidjan ulioko Kusini, na mamia zaidi waliuawa katika mji wa Magharibi wa Duekoue.
Gbagbo alikana mashtaka dhidi yake akieleza kuwa yalikuwa yamechochewa kisiasa na watu waliounda njama za kumuondoa madarakani.
Jopo la majaji wa ICC limeeleza kuwa Mwendesha mashtaka ameshindwa kutoa ushahidi wa kutosha kumtia hatiani Gbagbo kwenye mashtaka aliyokuwa ameyataja ikiwa ni pamoja na mauaji, ubakaji na unyanyasaji wa kingono uliofanywa na majeshi yake.
Kwa mujibu wa Reuters, Jaji Cuno Tarfusser ameeleza kuwa Mwendesha mashtaka “ameshindwa kuonesha namna ambavyo hotuba za Gbagbo zilivyochochea kutokea kwa vurugu na makosa mengine ya jinai yaliyotajwa”.
Reuters imefanya mahojiano na baadhi ya wahanga wa vurugu za mwaka 2010 ambao wameeleza kusikitishwa kwao na kuachiwa kwa mwanasiasa huyo.
“Kesi yoyote ile kama itamhusu kiongozi aliyekuwa madarakani basi inakufa ikifika ICC, na hii inaharibu namna ambavyo watu wanaichukulia Mahakama hii na wanapoteza imani na chombo hiki cha kimataifa cha kutoa haki,” Mark Kersten, mwandishi wa kitabu cha Justice in Conflict anakaririwa.
Katika hatua nyingine, wafuasi wa Rais huyo wa zamani wameripuka kwa furaha katika mitaa ya Ivory Coast wakifurahia uamuzi huo wa ICC.