Ripoti ya hivi karibuni iliyotolewa na Shirika la Kazi la Umoja wa Mataifa (ILO), imesema Watu milioni 50 walikuwa wakiishi katika utumwa wa zama za kisasa hadi kufikia mwaka 2021.
Ripoti hiyo, ambayo imewashirikisha Wakfu wa Walk Free na Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM), iliyotolewa jijini Geneva nchini Uswisi, imesema makadirio ya hivi karibuni kupitia utafiti wao, yanaonesha kuwa kazi na ndoa za kulazimishwa zimeongezeka katika miaka mitano iliyopita.
Imesema, “Watu milioni kumi zaidi walikuwa katika utumwa wa kisasa mwaka jana 2021 na hivyo kufikia watu milioni hamsini ikilinganishwa na makadirio ya kimataifa ya mwaka 2016, Wanawake na watoto wanabaki katika mazingira magumu kupita kiasi.”
Aidha, kati ya watu hao milioni 50, milioni 28 walikuwa katika kazi ya kulazimishwa na milioni 22 wakiwa katika ndoa za kulazimishwa huku Mkurugenzi Mkuu wa ILO, Guy Ryder akisema, “inashangaza kuona hali ya utumwa wa kisasa haibadilikitavumilia ukiukwaji huu wa haki za binadamu.”
Hata hivyo, wafanyakazi wahamiaji wanaonekana kuwa na uwezekano mkubwa wa kuwa katika kazi ya kulazimishwa kuliko wafanyakazi wenyeji na Mkurugenzi Mkuu wa IOM anasema ripoti hiyo itasisitiza udharura wa kuhakikisha uhamiaji wote ni salama na wenye utaratibu na wa kawaida.
Taarifa hiyo inafafaua kuwa, utumwa wa kisasa unatokea karibu kila nchi duniani, na unapita katika misingi ya kikabila, kitamaduni na kidini, huku zaidi ya nusu (asilimia 52) ya kazi zote na robo ya ndoa zote za kulazimishwa zinaweza kupatikana katika nchi zenye kipato cha juu au cha kati.