Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Shirika la kazi duniani ILO watu milioni 470 duniani kote hawana ajira kabisa au wameajiriwa chini ya kiwango yaani hawana kazi inayowalipa vizuri kuwawezesha kuendesha maisha na familia zao kikamilifu ambapo katika idadi hiyo vijana wapatao milioni 267 hawana ajira kabisa.
Kwenye ripoti ya ILO iliyotolewa tarehe 20 January 2020 ambapo ripoti hiyo imefichua hali mbaya zaidi ya kutia wasiwasi, huku akiongeza kuwa kukosa kazi nzuri ya kufanya, kunachangia kuongezeka kwa makundi ya waandamanaji katika jamii na machafuko yanayotokea ulimwenguni.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, mkuu wa ILO, Guy Ryder amesema hali inazidi kuwa ngumu kwa mamilioni ya wale wanaofanya kazi, kuboresha maisha ya wengine kupitia ajira.
Amesema masharti katika soko la ajira yamechangia mmomonyoko wa umoja wa jamii kwa njia nyingi, akizungumzia maandamano makubwa kama ambayo yameshuhudiwa Lebanon na Chile.
Kwenye ripoti ya kila mwaka kuhusu ajira na tathmini ya jamii, Shirika la Kazi Duniani, ILO, limesema Mwaka huu, idadi ya watu ambao wamesajiliwa kuwa hawana ajira inatarajiwa kuongezeka kutoka milioni 188 mwaka uliopita hadi milioni 190.5.
Mnamo mwaka uliopita, zaidi ya watu milioni 630, ikiwa ni asilimia 20 ya idadi jumla ya wanaofanya kazi ulimwenguni, walitegemea kazi ya kijungu jiko, yaani kipato ni chini ya dola 3.20 kila siku
Ripoti ya ILO imeonyesha kuwa asilimia 60 ya nguvu kazi ulimwenguni kote kwa sasa ni wale wanaofanya kazi zisizo rasmi, ambapo malipo ni kidogo na hawapati marupurupu muhimu.