Idadi ya vifo vitokanavyo na tukio la kuteketea kwa moto kwa jengo moja refu (ghorofa) jijini London nchini Uingereza imeongezeka hadi kufikia watu 12, huku zaidi ya watu 78 wakiwa wamelazwa hospitalini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na jeshi la polisi jijini humo, watu nane kati ya waliolazwa wako katika hali mbaya zaidi na kwamba hadi kufikia jana watu 65 waliokolewa kutoka kwenye jengo hilo.
Vikosi vya uokoaji viliitwa katika jengo hilo usiku wa manane huku mamia ya watu wakiwa ndani ya jengo hilo lilipoanza kushika moto.
Diwani wa eneo la Notting Dale amesema kuwa kulikuwa na kati ya watu 400 hadi 600 waliokuwa wakiishi kwenye jengo hilo lililokuwa na nyumba 120 za makazi.
BBC imeripoti kuwa Meya wa London, Sadiq Khan amesema wazima moto walifanikiwa kufika ghorofa ya 12 pekee na kwamba baadhi yao walipata majeraha madogo.
Bado chanzo cha moto huo hakijafahamika, lakini vyombo vya dola pamoja na katibu mkuu wa chama cha wazima moto amesema kuwa uchunguzi juu ya tukio hilo utaanza mara moja.