Idadi ya vifo kutokana na ajali ya treni mbili za abiria kugongana Kusini mwa India imefikia watu 13, huku wengine 25 wakijeruhiwa katika Wilaya ya Vizianagaram iliyopo Andhra Pradesh.
Wizara ya usafirishaji ya nchini humo imesema, uchunguzi wa awali uligundua kuwa kosa la kibinadamu lililosababishwa na kutokusimamia ishara, ndilo lililosababisha ajali.
Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi aliandika kwenye X, zamani Twitter kwamba amezungumza na waziri wa reli wa shirikisho na kutoa pole kwa familia zilizopoteza ndugu zao na majeruhi wapone haraka.
Hata hivyo, Modi alitangaza fidia ya kifedha kwa familia za waliokufa kwenye ajali hiyo kwa kiwango cha rupia 200,000 ($2,260, €2,397), huku Serikali ikitoa magari ya wagonjwa kadri iwezekanavyo kwenye eneo la ajali na hatua zingine za kutoa msaada.
Ajali za treni ni za kawaida nchini India na mara nyingi hulaumiwa kwa kosa la binadamu au vifaa vya ishara vilivyochakaa ambapo Mwezi Juni, kosa katika mfumo wa ishara za kielektroniki lilisababisha treni kubadilisha njia kimakosa na kugongana na treni ya mizigo katika jimbo la Odisha Mashariki.
Ajali hiyo iliwaua zaidi ya watu 280 na ilikuwa moja ya ajali mbaya zaidi ya nchi hiyo kwa miongo kadhaa na zaidi ya watu milioni 12 hupanda treni 14,000 kote nchini India kila siku, wakisafiri kwenye kilomita 64,000 (maili 40,000) za reli.