Idadi ya watu waliopoteza maisha kutokana na tetemeko la ardhi pamoja na tsunami vilivyokikumba kisiwa cha Sulawesi nchini Indonesia imeongezeka hadi watu 832.
Wakala wa kuthibiti majanga nchini humo imeeleza kuwa madhara ya majanga hayo yamekuwa makubwa zaidi ya namna ambavyo walikuwa wakifikiria awali.
Mamia ya watu waliripotiwa kukwama kwenye majengo yaliyoanguka Ijumaa ya wiki hii kufuatia tetemeko hilo lenye magnitude 7.5, kwa mujibu wa msemaji wa Wakala hiyo, Sutopo Purwo Nugroho.
Alisema kuwa tetemeko hilo lilisababisha tsunami yenye mawimbi ya urefu wa mita 6 yaliyowaua watu waliokuwa wanaendelea na shughuli zao ufukweni mwa bahari pamoja na nyumba nyingi zilizokuwa katika kisiwa hicho.
Taarifa zilizotolewa leo zimeeleza kuwa zaidi ya watu 1,600 wameathiriwa moja kwa moja na tukio hilo na maelfu ya makazi yameharibiwa vibaya.
“Hili tayari ni janga, lakini lingeweza kuwa na madhara makubwa zaidi,” taarifa ya Shirika la Msalama Mwekundu imeeleza.
Rais wa nchi hiyo, Joko Widodo aliwasili katika eneo la Palu na kuangalia madhara yaliyotokea. Alitembelea pia ufukwe wa Talise na kujionea uharibifu mkubwa uliosababisha maafa.