Katibu wa Chama cha Mapinduzi CCM Idara ya wazazi mkoa wa Njombe, Juma Nambaila kupitia ziara za viongozi wa chama hicho mkoani Njombe amezungumza na wanachama wa Idara yake ya wazazi akitoa maagizo na ushauri kwa wazazi mkoani humo kuelimisha vijana ili wafuate mila, desturi na maadili ya kitanzania.
Akizungumza kwa nyakati tofauti na wanachama wa CCM katika wilaya za Makete, Ludewa na Wanging’ombe mkoani humo, amesema kuwa Idara ya wazazi mkoani ina jukumu kubwa la kuelimisha jamii hasa vijana ambao mara nyingi wamekuwa na tabia tofauti na maadili ya kitanzania.
‘’Idara ya wazazi tuna jukumu kubwa la kuwaelimisha vijana wetu ili wajue kuwa chama hiki ni baba na mama yao maana vijana hawa wamezaliwa katika utawala wa chama cha mapinduzi leo wanapo kengeuka na kupita njia za tofauti sisi wazazi ndio tuwaelekeze wabadilike maana yawezekana hawajapewa maelekezo sisi tutimize wajibu wetu,’’amesema Nambaila
Aidha, ameongeza kuwa ili jamii iweze kusimama katika misingi imara inategemea zaidi uchumi imara wa vijana hivyo vijana wasipopewa misingi ya maisha kuanzia nyumbani kwa wazazi wao hawataweza kubadilika wakiwa mitaani maana huko wanakutana wakiwa na tabia za kihuni.
Hata hivyo, amewataka wazazi wa watoto wakiwa nyumbani wahakikishe kuwa wanatoa historia ya Chama cha mapinduzi CCM kwa watoto wao ili wanapo endelea kukua wakue katika misingi ya kujua historia ya ukombozi wa Tanzania umetokana na msingi madhubuti ya Chama cha mapinduzi kupitia Muasisi wa taifa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.