Mwenyekiti wa tume ya Uchaguzi Kenya, IEBC, Wafula Chebukati amesema kumeongezeka matukio kadhaa yaliyothibitishwa na kubainisha kwamba baadhi ya wapiga kura nchini humo wamekubali kuuza vitambulisho vyao vya kupigia kura kwa kulaghaiwa na kiwango cha pesa.
Chebukati amesema hayo zikiwa zimebakia siku chache kuelekea uchaguzi Mkuu nchini Kenya ambapo alikuwa akizungumza na Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai, kwenye ofisi yake kuhusu mwenendo wa Kampeni na namna Tume ilivyojipanga.
“Tumetoa habari hizo kwa maafisa wa polisi. Ninawaomba wapiga kura, tafadhali msiuze haki yenu ya demokrasia ya kuwachagua viongozi mnaowataka.
Chebukati alisema kwamba kuna watu waliokuwa wakizunguka kutafuta wakenya wanaotaka kuuza vitambulisho, ila hakutaja maeneo yaliyoathirika na tatizo hilo.
“Kuna watu wanaorandaranda kununua vitambulisho vya kitaifa kutoka kwa raia waliojiandikisha kuwa wapiga kura. Maelezo kuhusu habari hizo, yamewasilishwa kwa Inspekta Jenerali wa Polisi. “Hatua muafaka itachukuliwa dhidi ya wanaofanya biashara hiyo haramu. Ninatoa wito kwa wapiga kura kutouza haki yao ya demokrasia ya kushiriki uchaguzi mkuu ili kuwachagua viongozi,” Chebukati alisema.