Inspekta Jenerali wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu amefanya mabadiliko makubwa katika uongozi wa Jeshi hilo akiwahamisha na kuwapandisha vyeo  maafisa wa ngazi za juu nchini.

Mabadiliko hayo yamegusa maafisa waandamizi wa jeshi hilo waliopo katika makao makuu ya jeshi hilo na walioko mikoani.

Walioathirika na pangapangua ya IGP Mangu ni pamoja na Makamanda wa Mikoani, Wakuu wa Upelelezi wa Mikoa (RCO), wakuu wa Polisi wa wilaya (OCD), wakuu wa vikosi, wakuu wa polisi wa vituo (OCS) na askari wa vyeo vya chini.

Akizungumzia mabadiliko hayo, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Bulimba alisema kuwa mabadiliko hayo ni ya kawaida katika jeshi hilo na kwamba hayahusiani na ‘kasi ya rais Magufuli’.

“Mabadiliko hayo ni ya kawaida ya ndani, hayana uhusiano na kasi ya Rais John Magufuli lakini kazi lazima ifanyike,” Advera Bulimba aliiambia ‘Mwananchi’.

Kati ya waliobadilishwa ni pamoja na DCP Robert Boaz amehamishwa kutoka katika kitengo cha Intelijensia kuwa mkuu wa kitengo cha uhalifu wa kitaifa na uhalifu wa kupangwa, huku Kamishna Mwandamizi wa Polisi (SACP), Luteta Modest akihamishwa kutoka kitengo cha sheria kwenda kuwa mkuu wa kitengo cha sheria na huduma za utafiti.

Imeelezwa kuwa mabadiliko yaliyofanywa katika jeshi hilo ni makubwa na kwamba orodha ya waliobadilishwa ni ndefu kuliko orodha iliyoonekana awali kwenye mitandao.

Hivi karibuni, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alifanya mkutano na maafisa wa jeshi hilo katika Bwalo la Jeshi la Polisi liliko Oysterbay jijini Dar es salaam. Kati ya mambo yaliyozungumzwa ni pamoja na mpango wa kulifumua pamoja na kuongeza uwajibikaji.

 

 

Mchungaji Alazimishwa Kuoa ‘Maiti’ Ya Kiongozi wa Kwaya Aliyempa Mimba
Wamiliki wa Hotel Zilizoko Ufukweni Wapigwa Marufuku Hii