Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP. Camillus Wambura amewataka Watendaji wa Dawati la Jinsia na Watoto kutoa huduma bora kwa wahanga wa vitendo vya ukatili wanaoripoti matukio ya ukatili katika vituo vya Polisi ili kujenga taswira chanya ya Jeshi la Polisi kwa jamii jambo ambalo litasaidia kutoa haki kwa Wahanga wote wa matukio hayo.
IGP Wambura, ameyasema hayo Jijini Tanga wakati akifunga Kikao cha Watendaji wa Dawati la Jinsia na Watoto kutoka mikoa ya Tanzania bara na Zanzibar kilichokuwa kikifanyika jijini humo kwa siku tatu kwa lengo la kufanya tathmini kwa mwaka 2022 na kuweka mikakati kwa mwaka 2023.
Amesema “Kwa Takwimu zilizopo bado watendaji mna kazi kubwa ya kufanya huko mikoani kwa kuendelea kutoa elimu na kutowaonea huruma na muhali wahalifu wote wa vitendo vya ukatili wa kijinsia” Alisema IGP Wambura.
Kwa upande wake Kamishna wa Polisi Jamii, Faustine Shilogile alisema kikao hicho hufanyika kila mwaka kwa lengo la kufanya tathmini na kubaini mafanikio na changamoto ambazo huwekewa mikakati ili kuendelea kukomesha vitendo vya ukatili nchini.
Amesema Kumekuwepo na changamoto mbalimbali katika utendaji wa madawati nchini ikiwemo ukosefu wa majengo yenye vigezo vya Dawati katika baadhi ya vituo vya Polisi ambapo kwakushirikiana na wadau wataendelea kuboresha katika eneo hilo.
Awali, Mwakilishi wa Shirika la LSF, Bi. Jane Matinde alisema shirika hilo litaendelea kufadhili mafunzo kwa watendaji hao ili kuwa na watendaji wenye weledi katika dawati ambalo limekuwa mkombozi kwa wanajamii wa Tanzania ambao wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya ukatili.