Inspekta Jenerali wa Polisi Tanzania (IGP), Simon Sirro ameagiza kijana anayeonekana kwenye video iliyosambaa mtandaoni akiwatishia wenzake na bastola kujisalimisha katika kituo cha polisi.
IGP Sirro amewaambia waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuwa kijana huyo ameshapewa amri ya kujisalimisha lakini amekuwa ‘akipiga chenga’.
“Sisi tunatoa vibali vya silaha vinavyoambatana na masharti yake. Mtu anayepewa kibali cha kumiliki silaha lazima akidhi masharti hayo,” alisema IGP Sirro.
Ingawa kumekuwa na taarifa nyingi mitandaoni zikieleza kuhusu kijana huyo kujihami dhidi ya waliomtishia, IGP Sirro amesema kuwa watazifahamu sababu zote baada ya mtu huyo kufika kituo cha polisi na kuhojiwa.
Taarifa zilizoko mitandaoni zimekuwa zikimtambulisha kijana huyo kwa jina la ‘Shabani’, wengi wakieleza kuwa ni mume wa mtangazaji maarufu aliyekuwa Clouds TV na sasa anafanya kazi kwenye kituo chake binafsi cha habari kinachoruka mtandaoni (Online TV).
Mtu mmoja maarufu aitwaye Juma Lukole, alieleza kuwa Shabani alikuwa anajihami dhidi ya madereva wa malori ambao walikuwa wamezuia njia. Alisema wakati wa mabishano watu hao watatu walitoa panga na ndipo yeye akaamua kuwatolea bastola.
Hata hivyo, ukweli wa tukio hilo na utambuzi wa mhusika viko mikononi mwa Jeshi la Polisi. Tutakujuza taarifa rasmi zitakapotolewa.