Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, (IGP) Simon Sirro amefunguka na kusimulia kisa cha mapenzi kilicho wahi kumpata cha kuachwa na mchumba msomi kimyakimya baada ya kumtambulisha kwao.
Sirro mzawa wa Butiama mkoani Mara amesema aliachwa na mchumba wake waliyekutana chuo kikuu na kukubaliana kuoana kisha akamfikisha nyumbani kwao kumtambulisha.
Amesema baada tu ya kumtambulisha mchumba huyo alitokomea kimyakimya bila kumwambia, lakini alikuja kubaini sababu kubwa ilikuwa ni sifa mbaya za ukatili wa wanaume wa mara ndizo zilimkimbiza.
Ilimlazimu kusimulia kwa hisia mkasa huo wakati wa uzinduzi wa kituo cha Polisi cha Dwati la kijinsia na watoto cha Mugumu, Wilaya ya Serengeti kilichojengwa na UNFPA.
Sirro ametahadharisha kuwa vitendo vya ukatili vinafanya watu wasioe “Watu wanaogopa, mimi niliachwa na mchumba msomi wa sheria kimyakimya hili si jambo jema”
Amesema wanaume wa mkoa huo kuendekeza mifumo dume inayokinzana na mabadiliko ya kiulimwengu inasababisha madhara makubwa kwa wanawake, watoto na makundi mengine.
Na kuongeza kuwa suala la mahari kubwa kwa mkoa huo linachangia ukatili wa kijinsia kwa watoto wa kike, kwani wazazi hawafanyi kazi badala yake wanategemea kuoza watoto ili wapate ng’ombe wanaogeuka fimbo kwa binti.
Aidha amebainisha kuwa kwa sasa kuna ofisi za dawati 420 kwa nchi nzima kwenye vituo vya daraja A,B,C hivyo askari wanatakiwa kushughulikia makosa hayo kwa usiri mkubwa ili mhanga wa ukatili asionekane ananyanyasika tena.