Inspekta Jenerali wa Polisi, IGP Simon Sirro amemtaka dereva aliyekuwa na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu aliposhambuliwa kwa risasi afike katika kituo cha polisi ili kusaidia kukamilisha uchunguzi wa tukio hilo.

IGP Sirro ambaye yuko Mkoani Mtwara akifanya ziara yake ya kikazi amesema kuwa anashangazwa na maelezo yanayotolewa kuwa dereva huyo anapatiwa matibabu ya kisaikolojia nchini jijini Nairobi wakati anamuona akihojiwa na magazeti.

“Yule kijana kwenye picha ukimwona yuko vizuri tu, sasa wanaposema anapata huduma ya kisaikolojia wakati kwenye magazeti anaonekana, hii inatupa changamoto,” alisema IGP Sirro na kuongeza kuwa dereva huyo akifika Polisi atasaidia kupata majibu ya mambo mengi kuhusu tukio hilo.

“Mtu anasema anatibiwa kisaikolojia lakini kila siku nikiona kwenye magazeti anaonekana anawaka, inanipa tabu,” IGP Sirro anakaririwa.

Alieleza kuwa jeshi hilo lina uchungu na Lissu na linamheshimu kwakuwa ni mtu muhimu kwa Watanzania na kwamba wanataka kuwapata wote waliohusika na tukio hilo lakini wanahitaji ushirikiano ili kufanikisha.

Lissu anaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya Nairobi nchini Kenya baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 ambapo risasi tano kati ya hizo zilimpata. Tukio hilo lilitokea nyumbani kwake Area D mjini Dodoma alipowasili kutoka bungeni.

IGP Sirro awaomba wananchi kusaidia kumpata aliyemtishia Nape kwa bastola
Kundi la P-Square bado hali si shwari, Paul aibua mapya