Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro amesema vikundi vinavyotaka kuharibu amani katika uchaguzi jijini Arusha vitakamatwa kabla ya siku ya uchaguzi ili kuondoa malengo yao ya kuharibifu wa amani.

Sirro amesema hayo wakati akizungumza na askari polisi mkoani Arusha ambao wamepangiwa kusimamia amani katika uchaguzi keshokutwa.

Amesema polisi wamejipanga kuhakikisha hakuna vurugu ambazo zitatokea katika uchaguzi mkuu mwaka huu.

“Arusha imekuwa na historia ya vurugu sasa tumeleta polisi wa kutosha kudhibiti wachache wanaotaka kufanya vurugu,” amesema.

IGP amesema askari wanatakiwa kuhakikisha uchaguzi wa mwaka huu unakuwa wa amani  kwa kutokutokea changamoto yeyote ya kiusalama.

Sirro ameendelea kusema kuwa jeshi la polisi kwa kushirikiana na wananchi watahakikisha vikundi vya uhalifu vinachukuliwa hatua kwa haraka ili kusaidia wananchi waendelee kuishi kwa amani katika uchaguzi huo.

“Hatuwezi kuona watu wachache wanaotaka kuharibu amani, tutaomba hata nyinyi waandishi wa habari mtusaidie kutoa taarifa endapo mtawasikia ili wachukuliwe hatua kwa haraka.”

Jumla ya askari 710 wakiwemo  jeshi la polisi, Magereza, Uhamiaji, Zimamoto na Mgambo wamepangwa kwenda kusimamia uchaguzi wa mwaka huu.

Chanzo: Gazeti La Mwananchi

Sure Boy, Chirwa kuikosa Mtibwa Sugar
Kiongozi wa Al-Qaeda auawa Afghanistan