Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro ameeleza msimamo wa Jeshi hilo kuhusu maelekezo yaliyotolewa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dkt. Dorothy Gwajima, kumkamata na kumfungulia mashtaka Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima ambaye pia ni Mbunge wa Kawe, Josephat Gwajima.
Waziri Gwajima alitoa maelekezo hayo jana katika Kijiji cha Kyatunge wilayani Butiama mkoani Mara, akieleza kuwa Askofu Gwajima alitoa taarifa za kupotosha kuhusu chanjo ya corona iliyoingia nchini, pamoja na kuwatuhumu viongozi wa Serikali kuwa walipewa pesa kuipitisha.
Akizungumza na Ayo TV, IGP Sirro ameeleza kuwa jeshi hilo linasubiri maelekezo ya maandishi kutoka Serikalini ili liangalie kama kuna kosa la jinai au la, na kwamba endapo watakuta hakuna kosa la jinai wataishauri Serikali kutumia njia nyingine.
“Tumeyasikia hayo maelekezo, na maelekezo ya Kiserikali huwa mara nyingi yanakwenda kwa maandishi. Kwahiyo tunasubiri maandishi kuonesha kuna kosa gani. Unajua sisi tunashughulika na makosa ya jinai. Kwahiyo tunasubiri maelekezo kutoka kwake na tutaona kama kuna makossa ya jinai tutachukua hatua, na kama tutaona hakuna jinai basi tutashauri njia nyingine itumike badala ya kulitumia jeshi la polisi,” amesema IGP Simon Sirro.
Alipoulizwa kuhusu hatua ambazo Jeshi la polisi limekuwa likiwachukulia baadhi ya watu kutokana na matamshi wanayoyatoa, IGP Sirro ameeleza kuwa jeshi hilo huangalia kama matamshi yaliyotolewa ni ya uchochezi au yanaingia kwenye makosa mengine ya jinai ndipo huamua kumkamata na kumhoji mhusika.