Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro, ameutaja mkoa wa Kipolisi wa  Kinondoni kama kinara wa uhalifu nchini ambapo matukio ya uporaji, uvunjaji wa kutumia nguvu na uporaji kwa kutumia pikipiki yameongezeka huku uhalifu mwingine mkubwa wa kutumia silaha za moto ukiwa umeshuka.

IGP Sirro amesema hayo jijini Dar es salaam, wakati akizungumza na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa, watendaji Kata, pamoja na watendaji wa vikundi vya ulinzi shirikishi ambapo amewataka watendaji wote kutimiza wajibu wao kwa kuhakikisha usalama unaendelea kuimarishwa.

Aidha, IGP Sirro ametoa muda wa wiki moja kwa viongozi hao kuhakikisha wanakomesha vitendo vya kihalifu kwa kushirikiana na watendaji wengine huku akitoa wito kwa mgambo kuacha kujiingiza kwenye vitendo vya rushwa.

Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Tegeta, Bwana Mohamed Mawala amesema kuwa, wataendelea kutekeleza wajibu wao kwa kuzingatia uzalendo, taratibu na kanuni na kuhakikisha maeneo yao na wananchi wanaowahudumia yanakuwa salama.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mlalakuwa Suleiman Masare, ameahidi kutoa pikipiki mpya kwa Kituo cha Polisi Chuo Kikuu itakayosaidia kurahisisha utoaji wa huduma za kipolisi kwa wananchi.

Kabla ya kukutana na watendaji wa serikali za mitaa, watendaji wa kata na watendaji wa vikundi vya ulinzi shirikishi, IGP Sirro alifanya kikao kazi na maofisa na askari wa Jeshi na kuwataka kuendelea kutimiza wajibu wao na kuwachukulia hatua kali wanaojihusisha na vitendo vya kihalifu.

Zuma akana mashtaka yote, kesi yapigwa kalenda
Wizara ya afya kufuatilia wajawazito wote nchini