Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Simon Sirro amewataka Makamishna wastaafu kuendeleza elimu ya polisi jamii pamoja na kutoa msaada wowote utakaohitajika kwa jeshi la hilo.
Ameyasema hayo mapema hii leo jijini Dar es salaam wakati wa sherehe za kuwaaga makamishna wastaafu zilizofanyika katika viwanja vya Chuo cha Maafisa wa Polisi kilichopo jijini humo.
Aidha, Makamishna walioagwa ni pamoja na Paul Chagonja, Hamdan Omar Makame na Kenneth Kaseke, ambapo amesema kuwa kazi waliyofanya wastaafu hao ni kubwa lakini kustaafu kwao sio mwisho wa kutumika katika jeshi la polisi.
“Upolisi ni taaluma kama zilivyo taaluma nyingine hivyo utaalamu hauzeeki na kwetu sisi tunaondelea kubaki Jeshini tutaendelea kufuata yale yote mazuri mliyofanya na nyie mnapokuwa nje ya utumishi endeleeni kutusaidia kwa mawazo na milango yetu ipo wazi ili kuhakikisha nchi inaendelea kuwa salama,” amesema IGP Sirro
Kwa upande wake, Paul Chagonja ambaye alikuwa Kamishna wa Oparesheni na mafunzo kwa muda mrefu amewaasa Maofisa na Askari kuendeleza tamaduni na maadili ya Polisi pamoja na kufanya kazi kwa weledi.
Hata hivyo, Sherehe hizo zimehudhuriwa na Viongozi mbalimbali kutoka vyombo vya ulinzi na usalama, Mkurugenzi wa Takukuru Kamishna, Valentino Mlowola, IGP Mstaafu Said Mwema, DCI Mstaafu, Robert Manumba na Kamishna Mstaafu wa Kanda Maalumu ya Dar Es Salaam, Suleiman Kova pamoja na maofisa na Askari Polisi.