Jeshi la polisi Nchini limetoa onyo kwa mtu au kikundi cha watu watakaojaribu kuhamasisha mikusanyiko isiyo rasmi au kuandamana kwa namna yoyote.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 2, 2021 Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Simon Sirro amesema kuwa, tuhuma dhidi ya Mbowe na wenzake ziko chini ya mamlaka ya Mahakama hivyo ni vema wakaacha mamlaka hiyo itimize wajibu wake.
“Kabla ya uchaguzi nilisema kuna watu wamejipanga kulipua vituo vya mafuta na kuua viongozi wa Serikali hao wanaaopanga kuleta vurugu wajue Mbowe ni binadamu tumempeleka mahakamani tuache Mahakama ifanye kazi yake.”
Aidha IGP Sirro amewahasa wananchi wasiingie kwenye mitego ya kuandamana kwa kufanya hivyo mwananchi atakuwa anavunja sheria za nchi itakuwa ni kuvunja sheria za nchi huku akisisitiza kutokulaumu Jeshi la Polisi endapo litachukua hatua juu ya mwananchi anaevunja sheria.
“Msiingie kwenye mtego habari ya kusema kuandamana unavunja sheria na ukivunja sheria usilaumu jeshi maana umeingia kwenye uhalifu jeshi halitakuacha,” Amesema IGP Sirro.
Amesisitiz kuwa jeshi la polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama vimejipanga vizuri na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watu hao.
Hata hivyo Sirro amewasihi sana viongozi wa kidini, viongozi wa asasi zisizo za kirai kutoingilia suala ambalo lipo chini ya Mahakama bali kuacha Mahakama ifanye majukumu yake juu ya Mbowe, kwani watambue kuwa Mbowe pia ni mwanandamu sio Malaika hivyo kukosea ni jambo la kawaida.
Julai 31 Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika aliwataka wanachama wote ndani na nje ya Mkoa wa Dar es Salaam kujitokeza katika mahakama ya Kisutu siku ambayo kesi ya Mbowe itatajwa.