Mwezi Agosti 2023, Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani lilitangaza kuwashikilia Watuhumiwa 354 waliohusika katika uhalifu wa makosa mbalimbali ya jinai, ikiwa ni pamoja na kukamata nyama ya Swala na Magamba 11 ya Kakakuona ambazo ni nyara za Serikali katika mwezi agosti mwaka huu.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, ACP Muhudhwari Msuya alisema walifanya misako na operesheni mbalimbali kwa lengo la kuzuia na kutanzua uhalifu kuanzia Agosti 1, 2023 hadi Agosti 31, 2023 na kufanikiwa kukamata watuhumiwa hao 354.
ACP Msuya alisema watuhumiwa 114 walikamatwa kwa makosa ya kupatikana na dawa zinazodhaniwa kuwa ni za kulevya ikiwa ni pamoja na Bangi viroba 7, Puri 60, Kete 791 na Mbegu za Bangi kg 5, Mirungi Kilo 5, Bunda 3 za mirungi.
Watuhumiwa wengine wanne walikamatwa kwa makosa ya kubaka na 6 kwa makosa ya uvunjaji na watuhumiwa 99 walikamatwa kwa tuhuma za kuwa na Gongo lita 368 na mitambo miwili ya kutengeneza Pombe ya moshi huku watuhumiwa 97 wakikutwa na Pikipiki 111 za aina mbalimbali zinazodhaniwa kuwa ni za wizi.
Aidha, Watuhumiwa watano walikamatwa kwa tuhuma za mali za wizi wa Ngombe 2 na Mbuzi 3, Wahamiaji haramu 3 toka nchi ya Ethiopia 1, Kenya 1 na Uganda 1 ambao wamefikishwa idara ya Uhamiaji kwa hatua za kisheria.
Kamanda Msuya alisema, mtuhumiwa mmoja alishikiliwa kwa kukamatwa na Mafuta ya kupikia madumu matano na mtuhumiwa mmoja ambaye alifikishwa TRA kwa hatua za kisheria na watuhumiwa 28 walikamatwa na mali mbalimbali zilizoibiwa katika matukio ya wizi na uvunjaji.
Matukio kama haya yamekuwa ni kawaida kuyasikia na si mageni masikioni au machoni pa watu, hayaishii tu katika Mkoa wa Pwani bali yanatukia sehemu nyingi nchini, uharamu wake na uwepo wa vyombo vya kisheria na mbali ya kuwa yanapigiwa kelele na hata watu kukamatwa, lakini kila uchao hayaishi.
Je, ninani wa kumuangushia jumba bovu katika jambo hili? bila shaka IGP Wambura, Serikali, vyombo vya Sheria na wote wanaohusika wataangazia eneo hili na kupata ufumbuzi kisha kulimaliza kama si kuliondosha kabisa.