Kupitia taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya Habari, imesema Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Camillus Wambura amewahamisha baadhi ya Makamanda wa Polisi kutoka katika nafasi zao na kuwapangia majukumu mengine.
Taarifa hiyo iliyotolewa hii leo Oktoba 20, 2022 imesema Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, SACP Ulrich Matei amepangiwa kuwa Mkuu wa Kitengo cha Polisi Wasaidizi na Kampuni Binafsi za Ulinzi nchini, ambapo anachukuwa nafasi ya Kamishna Msaidizi wa Polisi, ACP Issack Katamiti.
Aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, SACP Ramadhani Ng’anzi, amehamishwa kwenda kuwa Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani na aliyekuwa Mkuu wa Kikosi hicho Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, SACP Wilbroad Mtafungwa, anakwenda kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza.
Taarifa hiyo imezidi kufafanua kuwa, aliyekuwa Afisa Mnadhimu Mkoa wa Kipolisi Rufiji, Kamishna Msaidizi wa Polisi, ACP Protus Mutayoba, amekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rufiji, baada ya Kamanda wa Mkoa huo kuhamishiwa Mkoa wa Kipolisi Temeke hivi karibuni.