Kikosi cha Ihefu FC kimeendelea kujichimbia Wilayani Mbarali Mkoani Mbeya kikijiandaa na Mchezo wa Mzunguuko wa 20 wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Young Africans.
Miamba hiyo itakutana uso kwa macho Jumatatu (Januari 16) katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, huku Young Africans ikiwa na deni la kulipa kisasi cha kupoteza mchezo wa Duru la Kwanza, uliopigwa Uwanja wa Highland Estates, Mbarali.
Katika mchezo huo, Mabao ya Ihefu FC yalikwamishwa wavuni na Never Tigere na Lenny Kissu huku bao la Wananchi likifungwa na Yannick Bangala.
Afisa Habari wa Ihefu FC, Peter Andrew amesema kikosi chao kipo kwenye morali kubwa kutokana na matokeo mazuri waliyoyapata hivi karibuni.
“Kocha amekuwa akiwapa wachezaji mazoezi mara mbili kwa siku, hii yote ni sababu ya maandalizi ya mchezo huo na kabla ya kuondoka atapunguza na kufanya mara moja kwa siku”
“Tunatarajia kuondoka Ijumaa kwenda Dar es Salaam, ili tuweze kupata muda wa kutosha zaidi wa kujiandaa na mchezo huo ambao ni muhimu zaidi kwetu katika kupambana na kuondoka eneo tulilokuwepo,” amesema Andrew.
Baada ya Michezo 19 ya Ligi Kuu Tanzania Bara Young Africans imeendelea kusalia kileleni mwa Msimamo wa Ligi hiyo ikifikisha alama 50, ikifuatiwa na Simba SC yenye alama 44 na Ihefu FC inashika nafasi ya 13 ikiwa na alama 20.